Hii ni tafsiri ya matini asilia ya Kiajemi. Matini asilia kwa Kiajemi

بسم الله الرّحمن الرّحیم
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

اِنّا فَتَحْنا لَکَ فَتْحاً مُبیناً لِیَغْفِرَ لَکَ اللهُ ما تَقَدَّمَ مِن ذَنبِکَ وَ ما تَأَخَّرَ وَ یُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَیْکَ وَ یَهْدِیَکَ صِراطاً مُستقیماً وَ یَنصُرَکَ اللهُ نَصْراً عَزیزاً.
Hakika Sisi tumekufungulia ushindi ulio wazi, ili Mwenyezi Mungu akusamehe makosa yako yaliyotangulia na yanayokuja nyuma, na akutimizie neema yake, na akuongoze kwenye njia iliyonyooka, na Mwenyezi Mungu akunusuru kwa nusura yenye nguvu. (Qur'ani, Al-Fat'h 48:1-3)

Siku arobaini zimepita tangu kutendeka kwa mojawapo ya jinai kubwa kabisa za maadui wa Uislamu na Iran, na tangu kutokea kwa mojawapo ya misiba mizito zaidi ya umma katika historia ya taifa hili; msiba unaounguza moyo wa kuuawa shahidi kwa Kiongozi Mtukufu wa Mapinduzi ya Kiislamu, baba wa taifa la Iran, kiongozi wa Umma wa Kiislamu na kiongozi wa wapenda haki katika zama hizi, bwana wa mashahidi wa Iran na wa Mhimili wa Muqawama, Khamenei Mkuu, قَدَّس‌الله نَفسَهُ‌ الزَّکیَّه (Mwenyezi Mungu aitakase roho yake safi).

Ni siku arobaini sasa tangu roho tukufu ya Kiongozi wetu shahidi iwe mgeni katika karamu ya mawalii, wakweli na mashahidi katika ujirani wa ukaribu wa Mwenyezi Mungu; na sambamba na hilo au baada yake, kundi kubwa la masahaba, makamanda na wapiganaji wa Uislamu, pamoja na wananchi wanaodhulumiwa, kuanzia watoto wachanga wa siku chache hadi wazee, nao wamejaaliwa kupata neema hii adhimu.

Ni usiku na mchana arobaini tangu Mwenyezi Mungu Mtukufu amwite kiongozi wa umma huu kwenye miadi Yake; lakini safari hii, kinyume na yaliyotokea katika zama za Kalimullah (Nabii Musa), masahaba wa Kiongozi shahidi na umma wake walisimama kuinua haki na kukabiliana na batili, wakasimama imara kama milima isiyotikisika mbele ya Samiri na ndama wake, na wakawashukia wavamizi na Mafirauni kama lava ya moto.

Ni mchana na usiku arobaini tangu mabeberu wa dunia waondoe barakoa zao za udanganyifu na uongo na kudhihirisha sura yao mbaya na ya kishetani ya mauaji na dhuluma, uvamizi na uongo, kiburi cha kifirauni na mauaji ya watoto, pamoja na udikteta na ufisadi.

Lakini kwa upande mwingine, ni siku na usiku arobaini ambapo wana shupavu wa Khomeini Mkuu na wa Khamenei mpendwa shahidi, na wafuasi wa Uislamu safi wa Muhammad (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake), wamekuwepo katika viwanja, mitaa na ngome za mapambano kwa juhudi na ushujaa wa kupigiwa mfano, na licha ya madhara na hasara za shambulio la kinyama la adui, wamevigeuza vita vya tatu vilivyolazimishwa kuwa uwanja wa ushujaa wa Ulinzi Mtakatifu wa tatu. Taifa la Iran lililo na ufahamu na macho ya busara, ingawa lilionyesha kwamba limejaa huzuni kwa msiba mkubwa wa kumpoteza kiongozi wake shahidi, lakini kwa kuwaiga warithi wa moja kwa moja wa Ashura ya Husseini, liligeuza msiba huo kuwa ushujaa na maombolezo kuwa mashairi ya vita. Na yote haya yamemtia adui aliyejizatiti kwa silaha hadi meno katika mshangao na kukata tamaa, na yamewafanya watu huru wa dunia wastaajabu na kusifu. Safari hii ujinga na upumbavu wa mabeberu ulisababisha mwezi wa Esfand 1404 kuwa mwanzo wa sura mpya ya kupata nguvu na kupanda kwa jina la Iran na Mapinduzi ya Kiislamu, na bendera ya Iran ya Kiislamu ipeperushwe si tu katika ardhi ya nchi yetu, bali pia katika kina cha nyoyo za wapenda haki duniani.

Mnasaba huu ni fursa nzuri ya kumtambulisha kwa ufupi Kiongozi huyo Mtukufu. Tunazungumzia mtu ambaye, kadiri alivyokuwa mashuhuri, hakutambulika ipasavyo. Kila mtu anajua kwamba Kiongozi wetu shahidi alikuwa mwanachuoni wa fiqhi anayezielewa zama zake na mwenye busara, mpiganaji wa jihadi asiyechoka na imara kama mlima, alimu anayetenda kwa elimu yake na mcha Mungu, mtu wa dhikri, sala za usiku, unyenyekevu mbele ya Mola na tawassuli kwa nafsi takatifu za Maasumina (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote), na kutoka ndani kabisa ya nafsi yake aliziamini ahadi za Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa sifa zake nyingine ni mapenzi kwa Iran na juhudi zisizokoma za kuimarisha zaidi na zaidi uhuru wa Iran mpendwa, na sambamba na hilo alisisitiza umoja wa kauli na mshikamano wa kitaifa. Alitumia umri wake wote katika juhudi za kusimamisha mfumo wa Kiislamu, kuuimarisha na kuuendeleza, na wakati huo huo kwa mtazamo wake Jamhuri ya Kiislamu bila wananchi haikuwa na maana. Pamoja na mamlaka na uthabiti wake, alikuwa na sehemu kubwa ya umakini katika fikra na mtazamo wake kuhusu mambo. Alizipa uwezo wa nchi, hasa vijana, umuhimu maalumu. Aliipa elimu, teknolojia na maendeleo yanayotokana nayo umuhimu mkubwa. Aliziheshimu kwa namna ya pekee familia tukufu za mashahidi, majeruhi wa vita na wajitoleaji wapendwa. Katika nyanja mbalimbali alikuwa na uzoefu wenye thamani kubwa uliokusanyika, baadhi yake ukiwa wa miongo kadhaa, pamoja na sifa nyingine nyingi zinazounda orodha ndefu. Siku hizi katika baadhi ya vyombo vya habari kunazungumzwa mara kwa mara kuhusu sanaa yake, ufahamu wake wa sanaa na ulezi wake wa sanaa. Kipengele hiki, ingawa peke yake kinaweza kuipa haiba ya mtu thamani kubwa, na bila shaka kilikuwepo kwa Kiongozi wetu mpendwa kwa maana yake halisi na kwa kiwango cha juu kabisa, lakini kikilinganishwa na vipengele vingine vya nafsi yake na fadhila zake, kinaonekana kuwa kidogo. Mimi binafsi namjua kuwa na sanaa nyingi: sanaa moja kubwa yake ambayo haizingatiwi sana ni sanaa ya kulea na kujenga jamii kwa kuunda fikra, mitazamo na hisia za umati mkubwa wa watu na makundi ya kijamii.

Sanaa yake nyingine ilikuwa ni uanzishaji wa taasisi zenye malengo maalumu, ambao aliufanya hasa katika miaka ya mwanzo ya kipindi cha uongozi wake, akiitazama mipeo ya mbali.

Sanaa yake nyingine ilikuwa ni hatua ya kuuimarisha muundo wa kijeshi wa nchi, ambao taifa la Iran liliyaona na kunufaika na matunda yake chanya katika vita viwili vya hivi karibuni vilivyolazimishwa. Vilevile, uwezo wa ubunifu na uvumbuzi katika nyanja mbalimbali, ziwe za kielimu, kimkakati au za utungaji sera, ulikuwa miongoni mwa sanaa zake nyingine, ambao sehemu yake inaakisiwa katika uandaaji wa Sera Kuu za Mfumo. Na pia uwezo wa kuzalisha maana kupitia kubuni kwa wakati muafaka maneno na misemo mipya, ambayo kila mmoja ulizalisha na kubeba wingi wa maana, na kutokana nao ikazaliwa hotuba ya umma. Na miongoni mwa sanaa hizo, ni ile iliyopatikana kwa kusafishwa kwa roho yake tukufu katika shida, mitihani na majaribu, na kwa sababu ya subira na msimamo wake katika njia ya haki: sanaa ya kutabiri matukio ya mbali, kwani اَلمُؤمِنُ یَنْظُرُ بِنورِ الله (muumini huona kwa nuru ya Mwenyezi Mungu). Na sanaa nyingine ambazo haiwezekani kuzihesabu katika maelezo haya mafupi.

Sanaa na fadhila hizi zote hazikuwa na chanzo kingine isipokuwa inayaya maalumu za Mwenyezi Mungu na uangalizi maalumu wa Bwana wetu (Imam wa Zama) na mababu zake watoharifu (rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote). Huenda yale yaliyozivuta inayaya na uangalizi huo kwa mtukufu huyo yanaweza kufupishwa katika juhudi na jihadi yake isiyokoma na ya ikhlasi katika njia ya kuinua neno la haki. Lakini hasa, mbali na mashaka ya mapambano dhidi ya utawala msaliti wa Pahlavi, alinufaika sana na fursa nyingine maalumu katika njia ya kutekeleza wajibu wake, ambayo kwa kawaida watu wengi hawaijui. Ilikadiriwa kwamba Sayyid huyo kijana, mwenye kiu kubwa ya elimu na pia mpenda kutenda, wakati ambapo baba yake mtukufu alikuwa hatarini kupoteza uwezo wa kuona, baada ya miaka kadhaa ya kupiga magoti mbele ya walimu wa daraja la juu, aliacha fursa zote za dhahiri za maendeleo ya kielimu na mustakabali mzuri katika mji wa Qom, na kwa kutegemea fadhila za Mwenyezi Mungu akajitoa kumhudumia baba yake. Fadhila ya Mwenyezi Mungu kufuatia kujitolea huku ilidhihirika kwa namna ambayo ghafla Sayyid Ali Khamenei, kabla ya kufikia umri wa miaka thelathini, alichomoza kutoka Khorasan kama jua, na punde akahesabiwa kuwa mmoja wa nguzo za fikra na mapambano, na wakati huo huo akapata maendeleo makubwa katika elimu za kawaida pia; kiasi kwamba katika miaka ya hamsini (ya kalenda ya Hijria Shamsia), shirika la SAVAK lilimwita Khomeini wa Khorasan. Ni lazima nisisitize kwamba mchakato huu wa kupanda kwa ndani na kwa nje kwa mtukufu huyo uliendelea pia katika vipindi vilivyofuata. Sasa, kwa ajili ya kujifunza kutokana na mwenendo wa wakubwa, hasa haiba kama hii, inafaa sana tuifanye sifa hii ya kutakiana kheri kwa ikhlasi na kusaidiana kuwa mwenendo wetu; kwani sifa hii, pamoja na kuitazamia rehema pana ya Mwenyezi Mungu, ndiyo tofauti muhimu kati ya yule aliyesimama chini ya bendera ya haki na wale waliokusanyika kuzunguka bendera ya batili. Bila shaka kufuata mwenendo kama huu kutakuwa ni kufungua milango ya mbingu na kushusha aina mbalimbali za misaada ya Mwenyezi Mungu na ya ghaibu; kuanzia kushuka kwa mvua ya rehema hadi kumshinda adui, na hata maendeleo ya kielimu na kiteknolojia.

Katika siku hizi inasikika mara kwa mara kwamba makundi mbalimbali ya wananchi wapendwa, kwa haki na kwa majonzi, wanamkumbuka mtu huyo wa kipekee wa zama zake, na polepole sura nyingi zaidi za johari ing'aayo ya haiba yake tukufu zinadhihirika. Vilevile, azma ya kuiga vitendo maalumu vya mtukufu huyo polepole inaenea; miongoni mwa hayo, wananchi wetu wapendwa wamejifunza mafunzo mengi kutokana na ngumi yake iliyokunjwa wakati wa kuuawa kwake shahidi, na sasa ngumi hiyo hiyo iliyokunjwa imekuwa kwa baadhi yao aina ya nembo ya pamoja ya itikadi. Hivi ndivyo inavyothibitika tena kwamba athari ya shahidi ni kubwa kuliko ya mtu aliye hai, na kwamba sauti yake ya wazi katika kulingania tawhidi, kutafuta haki na kupambana na dhuluma na uharibifu, imekuwa na mwangwi mkubwa zaidi na ujumbe wake kupenya zaidi kuliko wakati wa uhai wake; na pia kwamba matakwa ya moyoni ya shahidi huyu mtukufu, yaani saada ya taifa hili na mataifa mengine ya Kiislamu, yamekaribia zaidi kuwa kweli kuliko hapo awali.

Ndugu zangu wa kiume na wa kike, wananchi wenzangu! Leo, na hadi kufikia hatua hii ya ushujaa wa Ulinzi Mtakatifu wa tatu, inaweza kusemwa kwa ujasiri kwamba ninyi, taifa shujaa la Iran, mmekuwa washindi wa uhakika wa uwanja huu.

Leo mapambazuko ya kuibuka kwa Jamhuri ya Kiislamu kama nguvu kubwa, na kuingia kwa ubeberu katika mteremko wa udhaifu, yamekuwa wazi mbele ya macho ya wote. Bila shaka hii ni neema ya Mwenyezi Mungu ambayo imetunukiwa taifa la Iran kwa baraka za damu ya Kiongozi wetu shahidi na mashahidi wengine waliovikwa sanda za damu, wananchi wanaodhulumiwa na maua yaliyochanwa ya shule ya Shajarah Tayyibah ya Minab, na kufuatia tawassuli na unyenyekevu wa wananchi wote mbele ya Mola na kuwepo kwao kwa jihadi katika viwanja, mitaa na misikiti, na kwa sababu ya kujitolea kusiko na mipaka, bila masimbulizi na kwa ikhlasi kwa wapiganaji wa Uislamu walio tayari kutoa roho zao katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC), Jeshi la Taifa, Kikosi cha Polisi (FARAJA), askari wasiojulikana na walinzi wa mipaka. Neema hii pia, kama neema nyingine yoyote, ni lazima ishukuriwe ili idumu na ikue, kwani لَئن شَکَرتُم لَأزیدَنَّکُم (mkishukuru, hakika nitawazidishia). Shukrani ya kivitendo kwa neema hii ni juhudi zisizokoma za kufikia Iran yenye nguvu.

Kile kinachoonekana kuwa cha lazima katika hatua hii ya sasa ili kufikia kaulimbiu hii na lengo hili la kimkakati la Kiongozi shahidi ni kuendelea kwa uwepo wa wananchi wetu wapendwa kama ilivyokuwa katika zile siku arobaini walizopitia. Uwepo huu ni nguzo muhimu ya hadhi ambayo Iran yenye nguvu sasa imejikita ndani yake.

Kwa hiyo, kwa kutangazwa kwa uamuzi wa kufanya mazungumzo na adui, isidhaniwe kwamba kuwepo mitaani si lazima tena. Bali, hata ikidhaniwa kwamba kwa dharura imefika zamu ya kipindi cha utulivu katika uwanja wa vita vya kijeshi, jukumu la wananchi wote wenye uwezo wa kuwepo katika viwanja, mitaa na misikiti linaonekana kuwa zito zaidi kuliko hapo awali. Bila shaka sauti zenu katika viwanja zina athari katika matokeo ya mazungumzo; kama vile idadi ya kustaajabisha na inayoongezeka ya mamilioni ya kampeni ya “Jan-Fada kwa ajili ya Iran” (Kujitoa Mhanga kwa ajili ya Iran) nayo ni miongoni mwa vipengele vyenye athari katika uwanja huu. Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kutokana na nafasi hizi na kuendelea kwake, matarajio yaliyo mbele ya taifa la Iran yanabashiri kudhihiri kwa zama tukufu, zenye kung'aa na zilizojaa izza, heshima na utajiri kwa ajili yao. Kiongozi wetu shahidi alipochukua jukumu la uongozi, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulikuwa kama mche uliopigwa majeraha mengi na maadui wa Uislamu na Iran, na bila shaka ulivumilia yote vyema. Lakini alipoacha kiti cha uongozi wa umma baada ya takriban miaka 37, aliacha nyuma yake mti mwema ambao mizizi yake ni imara na matawi na majani yake yametanda kivuli juu ya sehemu muhimu za eneo na dunia. Mwelekeo wa kufikia “Iran yenye nguvu zaidi na zaidi” unapitia njia ya umoja kati ya matabaka mbalimbali ya jamii, jambo ambalo alilisisitiza mara kwa mara. Sehemu kubwa ya umoja huu ilitimia katika siku hizi arobaini: nyoyo za watu zilikaribiana, barafu iliyokuwa kati ya matabaka mbalimbali yenye mielekeo tofauti ilianza kuyeyuka, wote walikusanyika chini ya bendera ya nchi, na siku baada ya siku idadi na ubora wa mkusanyiko huu unaongezeka. Wengi kati ya wale ambao bado hawajafikia uwepo wa namna hii, kwa nyoyo zao wako pamoja na wanaunga mkono kauli za umati ulioko viwanjani.

Siku hizi wengi wanapata uzoefu wa mtazamo wa kistaarabu kwa kukodolea macho mipeo ya mbali, na wanajijengea taswira ambayo si ya kufikirika, bali inayotegemea uhalisia wa sasa na wa baadaye. Hii ni sifa ambayo hadi muda mfupi uliopita ilionekana katika idadi ndogo ya watu ambao Kiongozi shahidi alikuwa kinara wao. Hivi ndivyo kila mtazamaji anavyotambua ukuaji wa haraka na wa kimiujiza wa taifa hili, na si bure kwamba katika siku hizi, hakimu mashuhuri wa zama hizi na mwanachuoni mtukufu wa fiqhi, anapozungumza nanyi kuhusu hadhi hii, mara nyingi kwikwi ya koo humzuia kuendelea na maneno yake.

Katika fursa hii hii nawaambia majirani wa kusini wa Iran kwamba mnashuhudia muujiza. Kwa hiyo tazameni vyema, elewani vyema, simameni mahali sahihi na zitieni shaka ahadi za uongo za mashetani. Bado tunasubiri jibu linalofaa kutoka kwenu ili tuwaonyeshe udugu wetu na nia yetu njema kwenu. Hili halitawezekana isipokuwa kwa kuwapa mgongo mabeberu ambao hawapotezi fursa yoyote ya kuwadhalilisha na kuwanyonya. Wote wanapaswa kujua kwamba, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, hakika hatutawaacha wavamizi waovu walioishambulia nchi yetu. Hakika tutadai fidia ya kila hasara iliyosababishwa, fidia ya damu ya mashahidi na diya ya majeruhi wa vita hivi, na hakika tutaupeleka usimamizi wa Mlango-Bahari wa Hormuz katika hatua mpya. Hatukuwa na hatutafuti vita, lakini kwa vyovyote vile hatutaacha haki zetu halali, na katika mwelekeo huu tunauzingatia Mhimili mzima wa Muqawama kama kitu kimoja.

Katika kipindi hiki, hadi kufikia hatua ya kupata kile kilicho chetu, kwanza, wananchi wote wajitahidi kuzingatiana ili matabaka mbalimbali yasiathirike sana na upungufu ambao ni athari ya kawaida ya vita vyovyote. Bila shaka upungufu huu, ambao baadhi yake upo kwa kiwango kikubwa zaidi upande wa adui wenu, kwa fadhila za juhudi za ndugu zenu wa kiume na wa kike katika serikali na taasisi nyingine, umesimamiwa kwa kiwango kikubwa.

Pili, ni lazima kulinda masikio yetu, ambayo ni dirisha la akili na moyo, dhidi ya vyombo vya habari vinavyoungwa mkono na adui au vinavyoenda sambamba naye. Bila shaka vyombo hivyo vya habari havikutakii kheri nchi na taifa la Iran, na jambo hili limethibitika mara nyingi. Kwa hiyo, ama tuache kabisa kuvifuatilia na kuvitumia, au angalau tushughulike kwa shaka kubwa na kila kitu wanachowasilisha.

Tatu, ingawa taifa pendwa, kwa kumalizika kwa kipindi rasmi cha maombolezo ya kuuawa shahidi kwa Kiongozi wake Mtukufu, linavua nguo za maombolezo, lakini linaiweka hai ndani ya roho na moyo wake azma thabiti ya kulipiza kisasi damu yake safi na ya mashahidi wote wa vita vya pili na vya tatu vilivyolazimishwa, na litaendelea daima kuvizia kutimia kwa jambo hilo.

Mwisho, nikimhutubia Bwana wetu (Imam wa Zama), عجل‌ الله تعالی فرجه الشریف (Mwenyezi Mungu Mtukufu aharakishe faraja yake tukufu), nasema kwamba sisi, kwa imani kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa tawassuli kwa Maimamu Maasumina (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao), na kwa kumuiga Kiongozi wetu shahidi, tumesimama chini ya bendera yako mbele ya kambi ya ukafiri na ubeberu, na katika njia hii tumetoa mashahidi wenye thamani kubwa kutoka matabaka mbalimbali kwa ajili ya izza na uhuru wa nchi na kuinuka kwa Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu, na tumepata pia hasara nyingine. Sasa kwa nafsi zetu zote tunaitegemea dua yako maalumu kwa ajili ya ushindi wa uhakika dhidi ya adui, iwe katika uwanja wa mazungumzo au katika uwanja wa vita, na tunatumaini kwamba haraka iwezekanavyo, sisi na maadui zetu tutashuhudia athari yake ya kimiujiza, In sha Allah.

والسّلام علیکم و رحمةالله و برکاته
Amani iwe juu yenu, na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka Zake.
Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei
20 Farvardin 1405