Ujumbe kwa Mnasaba wa Kumbukumbu ya Kufunguliwa kwa Bunge la Kiislamu na Kuanza kwa Mwaka wa Tatu wa Shughuli za Bunge la Kumi na Mbili
Hii ni tafsiri ya matini asilia ya Kiajemi. Matini asilia kwa Kiajemi
بسم الله الرّحمن الرّحیم
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Nawapongeza wananchi wote wapendwa wa Iran ya Kiislamu na wabunge waheshimiwa wa Bunge la Kiislamu (Majlis-e Shura-ye Eslami) kwa Idi tukufu ya Kuchinja (Idul-Adh'ha) na kumbukumbu ya kufunguliwa kwa awamu ya kwanza ya Bunge la Kiislamu, na kwa mnasaba huu nazishukuru juhudi za wabunge, hasa Spika mheshimiwa wa Bunge la Kiislamu, Dkt. Ghalibaf, katika njia ya kuiinua nchi.
Bunge la Kiislamu ni kiini cha taifa, dhihirisho la demokrasia ya kidini na nguzo ya sheria na utungaji sheria katika Jamhuri ya Kiislamu, ambalo lina nafasi muhimu katika kutekeleza matakwa ya wananchi. Sasa, kwa kupita miezi mitatu tangu kuanza kwa Ulinzi Mtakatifu wa tatu, thamani ya ndani na kiini cha wananchi wa Iran katika imani, matumaini na matendo vimethibitika kwa rafiki na adui, na kupanda kwa kiwango cha wananchi wa Iran kumedhihirisha mwonekano wa kustaajabisha wa kiini cha fadhila za taifa.
Kwa kuwa mwakilishi halisi wa taifa anapaswa kuwa wa asili moja na taifa, kipindi hiki cha sasa ni hatua ya mabadiliko ya kudhihirika kwa mwamko wa wananchi ndani ya wabunge na Bunge la Kiislamu, ili wapange nafasi yao na utekelezaji wa majukumu yao katika kiwango cha taifa lililoamka, na kwa kazi na ubunifu maradufu, waharakishe na kuimarisha utungaji sheria na usimamizi katika njia ya kuweka reli za mustakabali wa Iran ya Kiislamu.
Katika uwanja huu wa jihadi, kiti cha ubunge kinahesabiwa kuwa kama ngome ya mstari wa mbele wa mageuzi katika njia ya maendeleo ya nchi. Kwa hiyo inafaa kwamba wawakilishi wa taifa, kwa kutegemea inayaya za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na Mtukufu, na kwa tawassuli kwa Bwana na Mola wetu (Mwenyezi Mungu Mtukufu aharakishe faraja yake tukufu), na kwa kuienzi damu safi ya mashahidi waliodhulumiwa wa vita viwili vilivyolazimishwa vya Marekani na Kizayuni, na wa kwanza wao Kiongozi wetu Mtukufu shahidi (Mwenyezi Mungu ainue daraja yake tukufu), kwa moyo wa jihadi watumie nguvu na uwezo wao wote kwa ajili ya utawala unaoshirikiana na kuongezeana nguvu na serikali na vyombo vingine, huku wakidumisha uhuru wa mhimili wa kutunga sheria, katika njia ya kuijenga upya nchi ipasavyo, kutatua mahangaiko ya wananchi hasa masuala ya kiuchumi na ya maisha ya kila siku, kustawisha uzalishaji na ajira, kukuza kiwango cha elimu na viwanda, kuinua utamaduni na maadili, kupambana na ufisadi wa kifedha, kudhibiti mfumuko wa bei na ughali wa maisha, na kuondoa umaskini kwa kila upande.
Kwa msingi huu, ni lazima maazimio ya Bunge yawe na uhusiano wa moja kwa moja na unaoonekana na masuala makuu ya nchi na mahitaji ya wananchi, na yaelekezwe katika kujenga matumaini na kuunda mustakabali wa nchi. Jamii, kabla ya kitu chochote, inahitaji kuona ishara halisi za matumaini, njia thabiti na taswira ya wazi ya mustakabali, ili iweze kupanga na kusonga mbele kwa msingi huo; na wabunge, kwa misimamo, maazimio na hotuba zao, wanaweza kulifanya Bunge la Kiislamu kuwa taasisi inayoongoza katika kujenga matumaini. Miongoni mwa hayo, katika hali ya sasa, kwa ushirikiano na mihimili ya utendaji na ya mahakama, na kwa kujikita katika kaulimbiu ya “Uchumi wa Muqawama chini ya kivuli cha Umoja wa Kitaifa na Usalama wa Kitaifa” katika mwaka 1405, wayafanye utulivu wa kiuchumi, kupunguza mfumuko wa bei, usimamizi wa ukwasi, kustawisha uzalishaji, kurekebisha Mpango wa Saba wa Maendeleo na kuongeza vipengele vinavyohusu ujenzi upya na ukarabati wa hasara za vita vya pili na vya tatu vilivyolazimishwa kuwa ajenda yao kuu, na wachore ramani ya njia ya harakati ya serikali na sekta nyingine katika hali ya sasa na kipindi cha baada ya vita.
Ili kutekeleza nafasi katika kiwango cha taifa lililoamka, maandalizi na mahitaji mbalimbali yanahitajika, ambayo katika fursa hii fupi, nawanasihi tu ndugu waheshimiwa wa kiume na wa kike kusoma kwa umakini na kwa uzito maelezo ya kina ya hotuba za Kiongozi Mtukufu shahidi (Mwenyezi Mungu ainue daraja yake tukufu) katika mikutano ya kila mwaka na wabunge wa Bunge la Kiislamu, hasa katika miaka ya hivi karibuni, ambazo zina thamani muhimu ya kiuzoefu na kiutendaji.
Ni jambo la kawaida kwamba kuzingatia uchamungu wa kibinafsi kuna nafasi ya msingi katika kuhakikisha kufuatwa kwa miongozo hiyo na utekelezaji sahihi wa majukumu mazito katika kipindi hiki nyeti; na miongoni mwa mahitaji haya ni: kutambua kwa usahihi vipaumbele, kura zinazotegemea tafiti na mashauriano ya kina ya kitaalamu, maisha ya kiwananchi na mawasiliano mapana na wananchi, kupambana na ufisadi kwa kila upande, kuyatanguliza maslahi ya kitaifa na madai ya umma kabla ya mahitaji na maslahi ya kimakundi, ya kivyama na ya kikanda, kuzingatia diplomasia ya kibunge, ushujaa na kutangaza misimamo ya wazi na yenye nguvu dhidi ya tamaa za kupita kiasi za mabeberu, na kuzingatia kwa busara na kwa moyo wa kimapinduzi nafasi mpya ya Iran katika eneo na dunia.
Miongoni mwa mifano ya uchamungu ni kuitunza neema adhimu ya umoja wa kitaifa na mshikamano usio na mfano ambao umetunukiwa taifa lililoamka kuzunguka bendera ya Iran ya Kiislamu, na ambao ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi za ushindi dhidi ya Shetani Mkubwa. Shukrani kwa zawadi hii ni juhudi za wananchi wote, hasa wasomi wa kifikra na kisiasa, wakiwemo wabunge, katika kulinda umoja huu na kujiepusha na mizozo tupu ya kisiasa na kukuza tofauti za kijamii.
Mpango na njama potofu ya adui baada ya vita vilivyolazimishwa, shinikizo la kiuchumi na mzingiro wa kipropaganda na kisiasa, ni kuzusha mifarakano na mgawanyiko wa kijamii ili kufidia kushindwa kwake katika uwanja wa kijeshi na kulipigisha magoti taifa; na ni lazima kila mmoja wa walio tayari kujitoa mhanga ambao nyoyo zao zinadunda kwa ajili ya Uislamu na Mapinduzi, au kwa ajili ya uhuru na heshima ya Iran, kuanzia sasa, zaidi kuliko hapo awali, wajitahidi kulinda umoja wa safu madhubuti na zilizoshikamana za taifa, wasizigeuze tofauti zisizo na sababu, na hata zenye sababu, kuwa mizozo na mifarakano, na kwa kauli na matendo wawe dhihirisho la mshikamano na umoja wa taifa, In sha Allah.
Nawatakia taufiki katika jukumu zito sana la kuwakilisha taifa lenye kustahili ambalo limesimama kifua mbele kukabiliana na dhuluma na uvamizi wa wanyama wakatili na waovu wa zama, na linaielekeza historia katika mwelekeo wake sahihi. Kwa matumaini kwamba dua ya Bwana wetu (Mwenyezi Mungu Mtukufu aharakishe faraja yake tukufu) itakuwa ni nguzo ya kuwaunga mkono, kuwaongoza na kuvuta taufiki za Mwenyezi Mungu kwenu, ninyi wapendwa.
والسّلام علیکم و رحمةالله و برکاته
Amani iwe juu yenu, na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka Zake.
Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei
7 Khordad 1405